Saturday, April 22, 2017

Njia Tano (5) Bora Za Kupata Mtaji Wa Kuanza Au Kukuza Biashara


Moja ya changamoto ambazo watu wengi wanaotutafuta huwa ni wanawezaje kupata mtaji wa kuanza biashara. Hiki kimekuwa kikwazo kwa watu wengi kuingia kwenye biashara. Hata wale ambao tayari wapo kwenye biashara, wamekuwa wakitamani kukuza biashara zao ila wanashindwa kutokana na kukosa fedha za kuingiza kwenye biashara.

Tatizo kubwa ambalo linawazuia wengi kutopata mtaji wa biashara ni kwa sababu inapokuja swala la mtaji wanafikiria sehemu moja tu, ambayo ni mkopo. Na kwa bahati mbaya sana watu wengi wanakuwa hawana sifa zinazowawezesha kupata mkopo wa kibiashara. Kwa kukosa sifa hizo huishia kukaa na kulalamika nataka kuingia kwenye biashara ila mtaji sina.

Kama wewe unapenda biashara, na umepanga kuingia au umeshaingia lakini hujaweza kukuza mtaji wako, hapa tutakupa njia mbalimbali za kupata mkopo kwa ajili ya biashara yako.


  1. Fedha zako binafsi.
Njia nzuri sana kwako kupata mtaji wa biashara ni kwa kuanza kuweka akiba ya fedha zako mwenyewe. Kama umeajiriwa anza utaratibu maalumu wa kuweka kiasi cha fedha pembeni ambacho hutakigusa hata iweje. Baadae unaweza kukitumia kwenye kuanza biashara. Kama hujaajiriwa unaweza kutafuta shughuli yoyote ukafanya na hii ikakuingizia kipato ambacho baadae utaweza kuanzia biashara.


  1. Michango kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki.
Kama unaweza kukaa chini na ndugu zako na ukawashawishi vizuri, watakuwa tayari kukuchangia uanze biashara. Kama watu wanaweza kuchangia harusi na mambo mengine, wanaweza pia kuchangia biashara, ni wewe uweze kuwashawishi vizuri. Ila hapa unahitaji kuwa unaaminika na ndugu hao n apia waoneshe ni jinsi gani wao watanufaika na biashara utakayoanzisha.


  1. Kutafuta mtu au watu wa kushirikiana nao.
Kwa uzoefu wetu, kuna watu wengi ambao wana mitaji ya kibiashara ila hawajui ni biashara gani wafanye au hawana muda wa kusimamia biashara. Na wakianzisha biashara kwa sababu hawana usimamizi mzuri wanapata hasara. Sasa wewe unahitaji kuwajua watu wa aina hii na andaa mpango ambao utawashirikisha na kuonesha ni kwa jinsi gani mkiungana pamoja mnaweza kuwa na biashara nzuri na yenye faida. Hii pia inahitaji uwe unaaminika na yule unayempelekea mpango wako.


  1. Kuanza biashara kwa fedha za mteja.
Hapa unaweza kukusanya fedha kwa wateja kwanza halafu ndio ukawapata huduma au bidhaa wanayohitaji. Kama utaweza kuwa na mpango mzuri wa biashara ambapo mteja anahitaji sana unachotoa, na tayari anakuamini anaweza kukupa sehemu ya gharama na wewe kutumia gharama hiyo kumpatia bidhaa au huduma anayotaka. Hii pia inahitaji uaminifu na wale unaofanya nao biashara.

Hii ndio njia ambayo inafahamika na kila mtu na watu ndio huwa wanaifikiria hii kila wanapofikiria mkopo wa biashara. Kama una sifa za kupata mkopo unaweza kuchukua mkopo na kuutumia kwenye biashara. Ila kuwa makini sana kama unachukua mkopo kwa ajili ya kuanzia biashara, ni hatari sana na unaweza kujiingiza kwenye matatizo zaidi.

Bado unafikiria ni njia gani unazoweza kutumia kupata mkopo wa biashara? Anza na hizo hapo juu na boresha kadiri biashara yako ilivyo na wale wanaokuzunguka walivyo. Hakuna kitu kinachoshindikana kama utaamua kweli kupata mkopo wa biashara.
 

No comments:

Post a Comment